Kwa ufupi
- Miili ya watu hao ilizikwa katika makaburi ya watakatifu wote baada ya ibada maalumu iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Anglikana la Watakatifu Wote mjini hapa.M
- azishi hayo yalihudhuriwa na maelfu ya waombolezaji kiasi kwamba kanisa hilo lilijaa na kuwalazimu wengine kukaa nje na eneo la makaburi.
Mpwapwa. Mji wa Mpwapwa jana uligubikwa na vilio wakati wa mazishi ya ndugu watano wa naibu waziri wa zamani wa viwanda, biashara, Gregory Teu waliofariki katika ajali iliyotokea nchini Uganda na kuua watu 13.
Miili ya watu hao ilizikwa katika makaburi ya watakatifu wote baada ya ibada maalumu iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Anglikana la Watakatifu Wote mjini hapa.
Mazishi hayo yalihudhuriwa na maelfu ya waombolezaji kiasi kwamba kanisa hilo lilijaa na kuwalazimu wengine kukaa nje na eneo la makaburi.
Wimbo maalumu wa kwaya ya Uvuke ya Kanisa la Anglikana la Roho Mtakatifu mjini Dodoma uliwagusa wafiwa na waombolezaji ambao wengi walionekana wakiangua vilio katika hiyo.
Katika ibada hiyo, Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dk Jacob Chimeledya alisema vifo hivyo viwe fundisho kwa waliobaki duniani kutenda mema.
Dk Chimeledya ambaye ni Askofu wa Dayosisi ya Mpwapwa, alisema hakuna haja ya kulalamika kuhusu vifo hivyo na kwamba huo ni mpango wa Mungu ambao unalenga kuwaimarisha waliobaki duniani kuishi maisha yanayompendeza yeye.
“Hakuna haja ya kusema huyu aliyeolewa kule ndiye amesababisha haya yote yatokee au huyu aliyeoa Tanzania ndiye amesababisha haya yote yatokee. Waliotwaliwa, wametwaliwa, tuliobakia tutengeneze maisha yetu. Msiba huu utuwezeshe kuyatenda yaliyo mema kwa sababu hatujui saa tutakapotwaliwa na bwana, yote haya tumuachie Mungu ni mpango wake anataka kutuimarisha katika maisha yetu duniani kwa kufanya yaliyo mema.”
Aliwataka kukesha kila wakati kwa kutengeneza maisha katika kila eneo mtu alipo kwa kufanya yaliyo makusudi ya Mungu.
“Kama ni kwenye biashara yako ukeshe kwa kufanya yaliyo mema, kama ni uongozi ufanye yaliyo kusudi la Mungu, kama ni kiongozi wa dini uwaongoze vizuri waumini ili waweze kuyafanya yaliyo mema,” alisema.
Alisema hakuna haja ya kufikiri kuwa tukio hilo lina mkono wa mtu, bali Mungu ameruhusu litokee kwa kuwa ana sababu nalo ambayo ni ushindi katika maisha ya watu wote.
Amewataka waumini kutafakari msiba huo kama fumbo ambalo halihitaji kutafakariwa pasipo Mungu.
“Tunatakiwa kuangalia kama Ayubu alipopata madonda na mateso yote hayo bado hakumuacha Mungu. Mungu alitupa kwa hiyo amechukua, kuna kupigwa na kuanguka tujiimarishe,” alisema.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria ibada hiyo ni Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye pia ni mbunge wa Kongwa na George Simbachawene wa Kibakwe.
Pia walikuwapo, naibu waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde ambaye pia ni mbunge wa Dodoma Mjini na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Suzan Kolimba
Baada ya ibada hiyo, Polisi kwa kushirikiana na askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), walifanya kazi kubwa kudhibiti umati uliokuwa umefurika katika Makaburi ya Vinghawe ili kuruhusu shughuli za mazishi kufanyika.
Kwa kiasi kikubwa shughuli za mazishi hayo zilisimamiwa na JWTZ kuanzia kuwasafirisha marehemu kutoka Dar es Salaam hadi Mpwapwa na wanajeshi pia ndio waliobeba miili ya marehemu hao katika maeneo yote.
Waliozikwa katika makaburi hayo jana ni George Teu, Alfred Teu, Paulina Ndagala, Sakazi Teu na Ester Teu.
Wakati wa ibada kanisani, maiti walikuwa sita lakini mwili wa Rehema Teu ulichukuliwa baadaye na ndugu wa upande alipoolewa kwa maelezo kuwa angezikwa baadaye leo katika makaburi hayohayo.

Comments
Post a Comment