Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya uhamiaji (IOM) limesema kuwa zaidi ya watu 60 wanahofiwa kupoteza maisha au kutoweka kufuatia boti iliyokuwa imewabeba waislamu wa Rohingya wanaokimbia mateso nchini Myanmar na kwenda Bangladesh kuzama. Msemaji wa shirika hilo linalohusika na masuala ya wahamiaji Joel Millman amewaeleza waandishi wa habari mjini Geneva kuwa watu 23 wamethibitika kufariki dunia baada ya miili ya watu wanane zaidi kupatikana usiku wa kuamkia leo. Millman amesema shirika hilo linakisia watu wengine 40 kutoweka baada ya boti hiyo iliyokuwa imebeba watu 80 kuzama. Afisa huyo wa IOM amesema hakuwa na taarifa za mara moja iwapo idadi ya watu wanaohofiwa kufa katika ajali hiyo itakuwa ndiyo kubwa zaidi tangu safisha safisha dhidi ya waislamu wa Rohingya ilipoanza nchini Myanmar August 25. Hadi sasa zaidi ya warohingya 500,000 wamekimbilia Bangladesh tangu safisha safisha hiyo ilipoanza.

Comments
Post a Comment